Rafiki Mwaminifu Na Wa Kweli Ni Yupi?

Masimulizi ...
by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Katika nchi moja ya ughaibuni alitokea Mfalme mmoja ambaye alioa wake wanne. Siku moja Mfalme aliugua kiasi kwamba alijiona anakufa, akaogopa upweke huko ahera.
Ilibidi awaulize wake zake swali moja lakini kila moja kwa wakati tofauti. Alianza na mke wa nne ambaye alikuwa anampenda sana, kupita wake zake wengine wote. Mke huyu alikuwa anamununulia vito vingi na vya thamani sana.
Mfalme alianza:
Mke wangu mpenzi, je nikifa leo uko tayari kufa nami na kufuatana nami ahera?
Mke wa nne alijibu:
“Samahani, haiwezekani hata kidogo, siwezi kufuatana nawe”, akaondoka zake.
Majibu ya mke wa tatu hayakuwa tofauti sana na yale ya mke wa nne, kwani alisema:
“Mimi ninayapenda sana maisha yangu, sitaweza kwenda nawe, ila itanipasa niolewe na mtu mwingine”.
Majibu ya mke wa pili yalikuwa hivi:
“Siwezi kwenda nawe ila nitakuandalia mazishi na nitayasimamia vizuri hadi mwisho, lakini sitafuatana nawe”.
Wakati anamjibu hivyo, ilisikika sauti ikisema:
“Nitaishi nawe milele katika raha na shida, hata kama ni maisha baada ya kufa”.
Mfalme aligundua kuwa aliyekuwa anaongea ni mke wake wa kwanza ambaye alikuwa hamjali wala kumtunza wakati akiwa na nguvu zake. Baada ya kutambua makosa yake, Mfalme alimwomba mke wake wa kwanza msamaha kwa kutomjali wala kumtunza kwa muda wote alioishi naye.
Mazungumzo haya yanatufundisha kuwa, kila binadamu ana wake wanne. Mke wa nne ni MWILI ambao huwa tunaugharamia na kuupamba kwa vito vya thamani na nguo za gharama kubwa lakini baada ya kufa hatufuatani na mwili huo.
Mke wa tatu ni MALI zetu ambazo tunajikusanyia kwa wingi lakini siku ya mwisho hatuwezi kufuatana nazo. Mali zote huwa zinaachwa na kugawiwa kwa ndugu wanaobaki. Hii ni sawasawa na mke wa tatu alivyosema kuwa ataolewa na mtu mwingine.
Mke wa pili anafananishwa na marafiki na familia zetu. Hawa watu huwa tunawathamini, tunawaamini na kuwapenda sana lakini nao pia hawawezi kwenda nasi zaidi ya kufika makaburini.
Mke wa kwanza ni ROHO zetu ambazo mara nyingi hatuzitilii maanani wala kuzijali. Roho ndizo pekee ambazo zitatufuata hata baada ya kufa.
Kwa hiyo tunaaswa kuijali miili yetu ili iwe na afya njema, kufurahia na kufaidi mali zetu tungali hai. Hali kadhalika, tuwathamini na kuwafurahia marafiki na familia zetu kwa upendo wanaotupa. Pamoja na hayo yote tukumbuke pia kutunza roho zetu kwa sababu roho ni chanzo cha maisha yetu na rafliki mwaminifu na wa ukweli.
Hata hivyo kuwa na marafiki wengi si hoja, hoja ni kuweza kuwachambua na kuwamudu. Hapa duniani tunapita na kila moja ataenda peke yake siku zake zikifika.
The Healing Hands Project
The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. . Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.
#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #ArtTherapy #Tanzania