Mwosha Huoshwa

Caroline Swai - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi ...

by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Huu ni msemo ambao hutumika sana katika jamii inayotuzunguka ukiwa na maana kuwa kama unamtendea mtu yeyote jambo baya, ukae ukijua kuwa iko siku nawe pia utalipiziwa kwa ubaya huo huo. Tupate kisa ambacho kinamhusu tajiri mmoja.

Hapo zamani za kale katika kijiji cha Zurii, alikuwepo tajiri mmoja ambaye alikuwa hana ushirikiano mzuri na wanakijiji wenzake. Katika kijiji hicho, kila ulipotokea msiba tajiri hakushiriki inavyopasa, badala yake alijitahidi kumwaga pesa kwa wenye msiba na kuondoka zake. Hata kulipotokea harusi kijijini hapo, vivyo hivyo alitoa hela bila kushiriki yeye binafsi au mwanafamilia kutoka nyumbani kwake. Pamoja na kutoshiriki katika misiba na sherehe mbalimbali, pia hakuwahi kushiriki katika vikao mbalimbali vya maendeleo ya jamii. Kama kawaida yake, alitoa hela na kuondoka zake.

Hali hiyo iliendelea kwa muda mrefu kiasi kwamba kila mwanakijiji aligundua na kujua kwamba familia ya tajiri haijishughulishi katika masuala yoyote ya pale kijijini.

Baada ya miaka kadhaa kupita, tajiri alifikwa na msiba mkubwa wa mke wake kipenzi. Wanakijiji walipopata tarifa za msiba, walifurahi sana na kushangilia wakiwa wanasubiri mwisho wake utakuwa nini. Kama kawaida, majirani na wanakijiji walishiriki lakini kwa lengo la kulipiza kisasi. Walimpelekea pesa na kuondoka haraka sana kama yeye alivyokuwa akifanya kwa wenzake wakipata matatizo / misiba. Jioni ndugu wa tajiri walikuja kwenye msiba wakakuta hakuna mwombolezaji hata mmoja, si jirani wala mwanakijiji. Walishangaa sana kuikuta hiyo hali. Ilibidi wamwuulize ndugu yao kulikoni.

Walianza: “Mbona hakuna waombolezaji katika msiba huu mkubwa namna hii”? Tajiri aliwajibu: “hata mimi sielewi kwa kweli. Majirani zangu na wanakijiji nafikiri wana matatizo, kwani kila anayekuja anaacha rambi rambi na kuondoka”. Tajiri alikuwa hajagundua wala kukumbuka kuwa chanzo cha shida ni yeye mwenyewe.

Ndugu zake waliona hapa kuna tatizo, hivyo wakajiongeza na kwenda kuwauliza viongozi wa kijiji. Ndipo walipojibiwa: “ndugu yenu huwa hahudhurii katika misiba, sherehe wala vikao vya wanakijiji wenzake. Kwa hiyo wanakijiji na majirani wanalipiza kisasi, wanataka ajifunze”.

Ndugu wakarudi kwa tajiri na kumweleza waliyoyapata kutoka kwa viongozi wa kijiji. Walimweleza bayana kuwa ana tabia mbaya ya kutoshirikiana na wanakijiji na majirani katika tukio lolote”. Kwa maelezo hayo tajiri aligundua tabia yake mbaya ya kutoshirikiana na wenzake katika shughuli mbalimbali za kijamii pale kijijini. Alichofanya tajiri ni kuwatuma ndugu zake wakamuombee msamaha kwa majirani na wanakijiji wote. Ndugu zake walifanya hivyo.

Wanakijiji na majirani walimsamehe na hatimaye wakashiriki katika shughuli yote ya mazishi. Tajiri alikiri na kuomba msamaha kwa dhati kwa wote aliowakosea na kuahidi kuwa atashirikiana nao kwa kila jambo, liwe jema ama baya.

Watu walisikika wakisema: “ Ama kweli, tajiri yamemkuta. Mwosha huoshwa.” Tajiri alipata funzo la kutosha na alibadilika na kuwa tofauti na alivyokuwa zamani.

Hapa tunapata funzo kuwa " usipende kumfanyia mtu kitu ambacho wewe hutopenda kufanyiwa, badala yake tujitahidi kushirikiana na jamii ili tusijenge uhasama kati yetu, hali ambayo inaweza kuleta kutoelewana, mtafuruku na hata ugomvi katika jamii".

Ni dhahiri kuwa , "umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu".

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Previous
Previous

Tuthamini Nyumbani Tulipotoka

Next
Next

Mkulima Mmoja, Walaji Wengi