Matatizo Katika Maisha Ni Mtaji

Simulizi
by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Mara nyingi matatizo katika maisha huleta maumivu makali kwa mtu yeyote na huwa yanakosesha amani hata kuweza kumfanya mtu apate msongo wa mawazo. Maumivu huweza kumfanya mtu achanganyikiwe.
Palikuwa na kaka mmoja ambaye alikuwa amefiwa na wazazi wake wote wawili. Akawa anaishi maisha ya mashaka mashaka. Akatokea ndugu mmoja ambaye aliamua kumchukua ili akaishi naye. Aliahid kumsomesha pia kama mtoto wake.
Ilitokea kuwa hali haikuwa hivyo ilivyotegemewa au kuahidiwa na msamaria huyo mwema. Maisha aliyokuwa akiishi yule mtoto yalikuwa ni ya mateso makubwa na wala hiyo ahadi ya kusomeshwa haikutimizwa. Kinyume chake alichokuwa anaambiwa ni kuwa yeye hatakiwi kusoma, wenye haki ya kusoma ni watoto wake tu.
Ilifika wakati hata kula ikawa ni shida kubwa kwake. Wakati wa kula yeye alikuwa anatumwa kwenda mahali, akirudi anakuta, aidha wamemaliza chakula ama kimebaki kidogo ambacho ndicho alitakiwa ale. Kama akikuta kimeisha hakutakiwa kuuliza, ilimlazimu kubaki kimya na kuumia ndani kwa ndani.
Hali ilizidi kuwa tete kwake na ilimbidi atoroke bila kujua anakoelekea. Mungu saidia, alikutana na mtu asiemjua na akamueleza shida yake. Yule baba aliamua kumchukua kwake. Aliishi naye vizuri na alimrudisha shule. Kijana alifanya vizuri shuleni. Alipomaliza shule, kijana aliandikishwa jeshini kwa ajira.
Kijana aliendelea vizuri kazini, akaanza kustawi vizuri na maisha yake yakawa mazuri. Waswahili husema, Mungu si Athmani. Kule ambako alikuwa amechukuliwa awali, ambako aliambiwa kuwa hakutakiwa kusoma, kulikuwa ni vurugu mechi. Hakuna mtoto hata mmoja ambaye alikuwa amefanikiwa katika ile nyumba. Badala yake wale ndugu zake waliokuwa na haki ya kusoma, walikuwa wakimuomba msaada awasaidie. Maisha kwao yalikuwa hayaeleweki, baba yao alikuwa amefilisika. Maisha ndivyo yalivyo.
Kijana alikuwa na moyo mkuu, moyo uliosheheni utajiri. Hakutaka kulipa mabaya. Aliwasaidia kadiri walivyokuwa wakiomba, bila kujali yaliyopita. Kwa hakika moyo wake ulikuwa wa kiungwana, moyo wa kijasiri.
Changamoto ama maumivu aliyoyapata, sasa yamebadilisha maisha yake. Mungu wetu hana choyo, alimpitisha kijana kwenye tanuru hiyo ya mateso ili aweze kukomaa na halafu akampatia kile alichokuwa amemuwekea. Kwa hakika, baada ya dhiki, faraja, wahenga walinena.
Tuna mengi ya kujifunza kwenye simulizi hii. Changamoto humwandaa mtu kwa maisha bora. Tunaaswa kuwa tunapokuwa na mapito magumu, kamwe tusikate tamaa. Hatujui Mungu ametuwekea nini huko mbele. Matatizo katika maisha ni mtaji wa mkubwa kwa maisha bora huko mbele. Yaliyompata huyu kijana yanasikitisha sana na yangeweza kumkatisha tamaa kijana. Lakini haikuwa hivyo. Yaliyompata baada ya taabu zote, yanafurahisha, yanafariji. Tunafundishwa kutokata tamaa hapa duniani kwani ni changamoto nyingi tu ambazo tutapambana nazo. Tuwe wavumilivu, tuwe na subira, kwani subira huvuta heri.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection