Matumizi Ya Teknolojia Ya Simu Yaleta Msaada Kwa Mama Na Mtoto

Simulizi
by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Katika kufanya kazi zake, "TEWWY" (Tap Elderly Women's Wisdom for Youth), haiko mbali na kauli mbiu ya Kimataifa na Kitaifa ya Siku ya Wanawake Duniani 2023. Kauli mbiu hiyo ya "Ubunifu na Mabadiliko ya Teknolojia, Chachu kuleta Usawa wa Kijinsia.” TEWWY inajitahidi kupunguza tofauti za kidigitali kati ya kizazi kipya na kizazi cha zamani kwa kutumia Teknolojia (simu) kutoa huduma kwa wanasihiwa wa jinsia zote.
Fuatana nami katika kisa hiki cha hivi karibuni na cha kweli kabisa.
Mama mmoja kutoka mkoa fulani alipiga simu akilia huku akiomba msaada wa unasihi. Alisema kuwa anadaiwa kulipa mkopo kwa Asasi fulani ya mikopo. Siku hiyo ilikuwa ni siku yake ya kupunguza deni lakini kwa bahati mbaya, alikuwa na shs 10,000/= tu za kurejesha wiki hiyo. Fedha hizo zilikuwa hazitoshi kufuatana na utaratibu wa marejesho uliowekwa. Huyu mama alimweleza mdai wake kuhusiana na mapungufu hayo. Mdai alimruhusu mdaiwa apeleke hicho kiasi cha shs.10,000/= alichokuwa nacho. Aliambiwa apeleke ofisini.
Wakati huo mtoto wa mgongoni wa mdaiwa alikuwa anaumwa na alikuwa na sindano za masaa. Hata hivyo, bila kuchelewa, alienda ofisini kupeleka hicho kiasi cha pesa alichokuwa nacho. Kumbe walikuwa wamemtegeshea, walikuwa wamemdanganya tu, ilikuwa ni njia ya kumnasa akifika huko ofisini.
Alipofika ofisini, badala ya Mdai kupokea kiasi hicho cha pesa, alimfungia ofisini pamoja na mtoto wake mgonjwa. Pamoja na kujieleza kote na kuwaomba wamwachie kutokana na mtoto wake kuwa ni mgonjwa anayehitaji dawa za masaa, maelezo hayo yaligonga mwamba. Hawakutaka hata kumsikiliza.
Bahati nzuri, mdaiwa alikuwa na simu ya Mnasihi mmoja aishiye Dar. Alimpigia simu na kumweleza yale yaliyomsibu. Mnasihi alichukua hatua ya kumtafuta Afisa Ustawi Jamii wa karibu na sehemu husika. Kwa bahati nzuri, Afisa huyu naye alichukua hatua haraka kwenda ofisini kwa Mdai. Aliwakuta mama na mtoto bado wamefungiwa.
Baada ya mazungumzo marefu, mama na mtoto walifunguliwa. Afisa Mikopo alichukuliwa hatua kwa kumfungia ndani mama na mtoto mgonjwa asiyekuwa na hatia. Mdai alifunguliwa mashtaka ya kuvunja haki za binadamu. Hivi sasa anasubiri kujibu kesi.
Kilichomponza mama huyo ni tabia yake ya kukopa bila malengo na kushindwa kurejesha pesa kwa wakati. Tabia ya kukopa kwa akina mama kila uchao imekuwa ni tatizo sugu. Akina mama wengi wana tabia ya kukopa kutoka asasi hii, kesho anakopa kutoka asasi nyingine ili kurejesha mkopo wa asasi aliyokopa huko nyuma. Kazi inakuwa ni kuhamisha mkopo kutoka asasi hii kwenda asasi nyingine. Tabia hii inawaweka akina mama wengi katika wakati magumu sana. Wanawake wengi wamejianzishia maisha magumu, maisha ya kuzikimbia nyumba zao ili wadai wasiwakute.
Mkasa huu unatufundisha nini?
Tunaaswa akina mama kuacha kukopa kopa bila malengo maalumu. Kukopa ni jambo la kawaida ila kile tunachokopa, yatupasa tufanyie kitu kitakachozalisha fedha zaidi ili tuweze kulipa deni na kutumia faida tuliyopata kuendeleza mradi. Kukopa kwa ajili ya kutunzana akina mama kwa sababu ya jambo moja ama jingine kuna athari kubwa mbeleni. Mathalani, kukopa kwa ajili ya ‘vijola’ ni hatari kwani kile ‘kijola’ hakiwezi kukuletea faida, hivyo hutaweza kurudisha mkopo huo. Akina mama, tuwe makini na mikopo isiyokuwa na tija. Mikopo imesababisha wengine hata kufikia hatua ya kujiua pale waliposhindwa kulipa. Hima akina mama, hebu tubadilike. Tukope kwa ajili ya vitu vyenye tija. Tuache tamaa, tuache kuiga. Tujitahidi kuishi maisha ya kawaida, maisha yasiyo na usumbufu huko mbeleni. Mikopo husababisha msongo wa mawazo pale unapokuwa huna njia ya kulipa.
Teknolojia ya simu ilimuokoa mama yule aliyekuwa amefungiwa kwenye ofisi ya mikopo. Tuendelee kuitumia teknolojia, inasaidia sana. Iliweza kumuokoa mama yule alyefungiwa ofisini kwa sababu ya kutorudisha fedha za mkopo. Akina mama kumbukeni, na wenyewe mumeona, mkopeshaji anakuja kwako kwa heshima na adabu. Anakuja na luggage tamu ya kulaghai na kukubembeleza ili ukope. Anapokuja kudai anabadilika kabisa, unafikiri siyo yule aliyekuwa anakubembeleza wakati akitaka ukope. Waogopeni sana watu hawa, kama huna mradi wa kuzalishia hizo pesa unazokopa, ni vema usikope kabisa.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection