Tuwe Na Roho Za Kiasi

Simulizi ...
by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Ni jambo la kupendeza sana ukiwa na roho ya kiasi. Siku moja, Fisi aliondoka nyumbani kwake ili akatafute chakula cha jioni. Kabla hajafika mbali, alimwona mtu aliyekuwa amedhoofika sana amefungwa kwenye mti. Huyu jamaa alikuwa amepitishiwa hukumu hiyo na wazee wa kijiji kutokana na vitendo vyake vya kinyama. Alikuwa mwizi, mnajisi na muuaji.
Mjumbe wa baraza la wazee wa kijiji alifika na kumcharaza viboko katika eneo hilo alilofungiwa mara tatu kwa siku, yaani asubuhi, mchana na jioni. Walitafutwa watu wenye nguvu ambao awali waliwahi kufanya kazi katika jela la wahalifu sugu. Wajumbe hawa walimtandika hadi akawa hoi, hajijui na hajitambui.
Fisi alipomkaribia huyu jamaa mkondefu alimwonea imani akamwuliza: “Vipi mwenzangu, kwa nini wamekufungia mtini? Isitoshe, inaonekana unatokwa na damu puani na mdomoni.” Jamaa alimeza mate kwa shida kisha akasema kwa sauti iliyodhihirisha maumivu makubwa aliyohisi. Alimwambia fisi kwa nini amedhoofu.
“Nimekataa kunywa supu ya mzoga wa Pundamilia. Supu yenyewe ilikuwa inanuka kweli kweli. Nisingeweza kuinywa hata wangenilenga mtutu wa bunduki utosini”.
Fisi akasema kwa uchangamfu, "Mimi nitainywa hiyo supu bila wasiwasi. Iko wapi?"
Jamaa akamwuuliza Fisi, “Ungependa kufungwa kwenye huu mti ili upate fursa ya kuinywa hiyo supu?"
Fisi akajibu haraka haraka: “ Bila shaka”.
Fisi alimfungua yule jamaa, kisha yeye akafungiwa mtini. Jamaa alipofunguliwa alitoweka, hakuonekana tena katika eneo hilo lilllokuwa limeshuhudia ukatili wake kwa muda mrefu. Usiku wa manane, mjumbe aliwasili akiwa na nguvu ya kutosha kumcharaza yule mhalifu. Kulikuwa na giza totoro. Bila kupoteza wakati, aliuinua mjeledi wake ukatua kwenye mgongo wa Fisi. "Chwaaaaaa!" Mwangwi wa kipigo hicho ulitawala msituni usiku huo.
Fisi alihisi maumivu ambayo hajawahi kuyapata maishani mwake. Ndipo akaanza kusema kwa sauti ya juu, “Nitainywa! Nitainywa yote”.
“Nini?” mjumbe akauliza kwa mshangao.
“Nitainywa hiyo supu, hata kama imejaa nzi.” fisi akasema.
Mjumbe aliendelea kumcharaza kwa nguvu zaidi. Fisi alipiga nduru hapo ndipo mjumbe alipogundua kuwa yule mhalifu alikuwa amemvisha fisi kilemba cha ukoka. Alimfungua Fisi na kumwomba msamaha.
Wazee wa baraza waliipokea habari hii kwa masikitiko makubwa.
Somo hili linatufundisha katika maisha yetu ya kila siku kwamba tusiingilie mambo ya wengine bila kujua chanzo chake vinginevyo tutajikuta tunapata matatizo ambayo hayatuhusu.
The Healing Hands Project
The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.
#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania