Turidhike Jinsi Tulivyo

Caroline Swai - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Mara nyingi, hususan wanawake, tuna kawaida ya kutoridhika na maumbile/muonekano wetu, yaani vile jinsi Mungu alivyotuumba. Haina maana tusijirembe, la hasha. Maana kubwa haswa ni kuwa tusimsahihishe Mungu vile alivyotuumba, bali tuuheshimu uumbaji wake. Kuna mifano kadhaa inaweza kutolewa, mifano ambayo ipo na itaendelea kuwepo kwani kila siku ipitayo tunashuhudia mambo mengi tu yakitokea na yanaendelea kutokea.

Kuna kijana mmoja ambaye ni mtoto wa Profesa kwenye chuo fulani hapa nchini. Wakati akiwa anasoma chuo alikutana na dada mmoja ambaye alikuwa mzuri wa sura, mrefu na mwembamba wa wastani. Dada huyu pamoja na kuwa mwanafunzi wa Chuo naye pia alikuwa mtoto wa Profesa. Wawili hawa walipendana sana hadi wakakubaliana kuoana pindi watakapomaliza chuo. Muda wa likizo uliwadia, chuo kilifungwa na hivyo kila mtu alirejea makwao.

Baada ya likizo kuisha, wanafunzi walirejea tena chuoni. Cha ajabu, yule dada alirudi akiwa amebadilika mno kimaumbile, kiasi kwamba alimvutia kila mwanachuo kumuangualia mara mbili mbili. Wengi walijiuliza, kimoyo moyo, kulikoni? Nini kimemsibu dada huyu? Mbona kabadilika sana? Ili mradi kila mwanachuo alijiuliza mwenyewe.

Ukweli ni kwamba kumbe dada huyu alikuwa hajaridhika na umbile lake la awali/asili, alikuwa akitamani makalio makubwa. Kwa hiyo wakati wa likizo alipata fursa ya kujitengeneza vile atakavyo, alimsahihisha Mungu kwa kuchoma sindano ya kuongeza makalio makubwa. Alifanikiwa na hivyo alipata kile alichokuwa akitamani siku zote. 

Pamoja na mabadiliko hayo, yule kijana hakuacha kumpenda msichana huyo. Mawazo yake yalibakia vile vile, Aliendelea kumpenda yule dada, na pengine, zaidi ya vile ilivyokuwa mwanzoni. 

Mara baada ya kumaliza chuo wawili hao walifunga pingu za maisha kwa sherehe kubwa na yenye kufana sana. Vijana hao waliendelea na maisha yao. Baada ya mwaka kupita, walibarikiwa kupata mtoto. Cha kushangaza lakini, dada huyu baada ya kujifungua, maumbile yake yalianza kubadilika kwa kasi. Alianza kunenepa vibaya kuanzia kiunoni, hususan, sehemu za makalio kiasi kwamba alianza kushindwa kunyanyuka. Unene ulizidi, ulikuwa wa kupindukia.

Wazazi wa pande zote walitafakari la kufanya ili waweze kukabiliana na hali hiyo. Hatimaye, walifikia muafaka wa kuchangishana pesa kwa lengo la kumpeleka nje ya nchi 

kwa matibabu. Tiba ya operesheni ilifanyika kwa gharama kubwa sana na hatimaye binti alipata nafuu. Walirudi nyumbani pamoja ja na mume wake kwani alikuwa amemsindikiza. 

Maisha yaliendelea lakini mume wake hakuwa na raha naye tena. Aliogopa kumpa mimba tena mke wake kwa lengo la kupata mtoto mwingine. Aliogopa na kuhofia matatizo yanayoweza kutokea tena baada ya kujifungua. Lakini ukweli ni kwamba, yaliyompata mkewe yalikuwa ni matatizo ya kujitakia. Kidogo kidogo, mume alianza kusononeka na matatizo yaliyomsibu mke wake. Alijikuta yuko njiapanda. Alifikia hatua ya kutaka kumuacha mke wake. Wazazi wa pande zote mbili waliona kuwa hili tatizo lilikuwa na muelekeo wa kusambaratisha ndoa ya vijana wao. Walijitahidi kuingilia kati ili wasiachane. 

Sote tunajua kuwa, hakuna mzazi anayependa ndoa za watoto wao zivunjike. Kwa ndoa hii, ilishindikana. Jitihada zao ziligonga mwamba. Kijana alifanya maamuzi magumu, alimuacha mke wake, akaoa mwanamke mwingine, wakiishi kwa raha mstarehe. 

Simulizi hii ni fundisho kubwa na zuri sana, hasa kwa akina dada wanaopenda kuikosoa kazi ya Muumba. Kuna tabia imejengeka sana kwa akina dada wengi ambao hufikiria kuwa uzuri wa binti uko kwenye makalio ama kujichubua. Mabadiliko yoyote yanayofanywa kwenye miili yetu bila ushauri wa daktari … ni HATARI TUPU ⚠️⚠️ ⛔️

Yatupasa turidhike vile na jinsi Mungu alivyotuumba. Ikumbukwe kuwa hakuna mwenye ubavu wa kumsahihisha Muumba wetu. Kama hatuna uwezo wa kuongeza urefu wa unywele hata kwa sentimita moja, tutawezaje kuongeza makalio kwa kuchoma sindano ama kutumia dawa? Jamani, tusidiriki kumsahihisha Mungu kwani madhara yake yanaweza kuwa makubwa sana. Kujipodoa ama kujiremba ni sahihi kabisa, lakini vinginevyo…..tuvikwepe, kwani haviko ndani ya uwezo wetu.

Turidhike jinsi tulivyo.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Previous
Previous

Chezea Mshahara, Usichezee Kazi

Next
Next

Faida Na Hasara Za Kuiga