Nyakati Ngumu Hutengeneza Watu Imara

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Kwa kawaida linapotokea jambo lolote hapa duniani, binadamu huishia kulaumu na kusikitika. Zaidi ya hapo huwa tunatoa maneno ya…kama ingefanyika hivi au ingekuwa vile haya yasingetokea. Chochote kile huweza semwa ili mradi tu cha kusema kiwepo kwani binadamu ndivyo tulivyo.

Mara nyingi, watu tunapenda sana kusema … ninge….. nisinge…. Ukiishaanza kusema, mathalani, ningelijua kuwa itakuwa hivi, nisingejiingiza huko, tayari inakuwa ni shida. Neno “nge” huwa halina maana kabisa wakati likisemwa kwani tayari jambo linakuwa limekwishatendeka.
Hii ina maana kuwa tunashindwa kuelewa kuwa kila jambo limepangwa sio kwa ubaya tu bali na kwa uzuri pia. Jambo zuri linaweza kutokea lakini pengine chanzo chake ni lile jambo gumu ambalo lilikuwa limetokea huko nyuma.

Hebu na tuangalie ajali ya ndege iliyotokea hivi karibuni ambapo watu wengi walipoteza maisha. Pamoja na kwamba mfano huu unaweza usiwe mzuri sana, hasa kwa wale waliopoteza ndugu zao lakini kwa kijana Majaliwa na ndugu zake, mfano huu utaleta maana tofauti. Majaliwa amejulikana kuwa shujaa kutokana na kazi kubwa aliyoifanya ya kuokoa wahanga wa ajali. Kijana Majaliwa, muanika dagaa mwaloni ameibuka na kuwa shujaa. Sasa Majaliwa amekuwa ni zungumzo nchini kote. Hakuna aliyetegemea kuwa muanika dagaa siku moja ‘angeukata’.

Pamoja na kwamba inauma sana, lakini msemo wa “Kufa Kufaana” unaweza kuleta maana hapa kwa upande wa Majaliwa na ndugu zake. Kuinuliwa kwa Majaliwa kumetokana na yeye kujitoa bila uoga na kuokoa watu 23, alijitoa kwa moyo wake wote. Uzalendo wake pia ulimtuma Majaliwa kujitoa kwa ajili ya binadamu wenzie waliokuwa hatarini. Kung’ara kwa Majaliwa ni ushindi kwa familia yake pia kwani nao wanainuliwa kutoka hali ya chini waliyokuwa nayo. Kutokana na simulizi zimhusuzo kijana Majaliwa, familia ilikuwa haina uwezo wa kumsomesha mtoto wao pamoja na kwamba kijana alikuwa na nia sana ya kusoma. Hakupenda kuishia maisha ya mwaloni kuanika dagaaa.

Kuna usemi usemao kuwa huwezi kufanikiwa mpaka usukumwe. Majaliwa amesukumwa na ajali ya ndege. Utayari wa Majaliwa kujitosa umeokoa roho za watu 23. Je unafikiri hao waliookolewa wanasema nini juu ya huyo kijana? Maombi yao yote kwa Muumba wetu yanaelekezwa kwake Majaliwa. Kuna maandiko ya vitabu vitakatifu yanasema, “Hutakufa kabla lile Mungu aliloweka ndani yako litimie.” Kwa wanaoamini andiko hili, ina maana kwamba Mungu hufanya kazi na mtu mmoja aliye tayari.

Lakini wakati upande moja unasherehekea kupandishwa daraja ya maisha yao, familia zilizopotelewa na wapendwa wao, zina majonzi yasiyo kifani😭😭 Ni vigumu sana kuupima uchungu walionao waliofiwa na ndugu zao, watoto wao, rafiki zao na jamaa wengi. Hebu tujiweke ndani ya viatu vyao. Ni uchungu ulioje huo. Hebu tuwafikirie na kuwaombea kipekee, hususan yule baba aliyepoteza watoto wake wawili kwa mpigo 😭🙆🏽‍♂️ INAUMA….INAUMA sana. Utawafarijije wafiwa hawa? Utamfarijije baba huyu? Ni ushauri nasaha gani utampatia ili aweze kuelewa kuwa “Bwana Ametoa, na Bwana Ametwaa?”

Sasa hebu tuje kwako wewe mwana Tewwy. Je uko tayari kwa ajili ya kufanya unasihi kwa watu wenye matatizo ya afya ya akili? Jibu linatakiwa liwe NDIO, kwani hiyo ndio kazi tuliyoikubali kuifanya kwa uwezo wetu wote kutokana na uhitaji wa watu uliopo. Yatupasa tujitahidi kwa sababu kazi tuliyo nayo ni kubwa sana. Inatupasa kujituma, malipo yetu mungu anajua. Tuwe tayari wakati wote ili tutengeneze uimara wetu na kuwa wanasihi wanaotegemewa hapa nchini. Tusikate tamaa na kuogopa tunapopitia magumu katika kazi yetu ya unasihi. Tukumbuke kuwa nyakati ngumu hutengeneza watu imara. Kazi iliyo mbele yetu ni kubwa sana, tunamuomba Mungu atutie nguvu ili tuweze kuendelea kuokoa watu wengi zaidi na zaidi. Watu wanatuhitaji kutokana na busara zetu alizotupatia Muumba wetu.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Previous
Previous

Muacha Asili Ni Sawa Na Mtumwa

Next
Next

Tuna Sababu Ya Kumshukuru Mungu