Ubaya Unavuma Kuliko Wema

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Usemi huu unatufundisha wale wote ambao tunapenda kuishi na ndugu kufuatana na mila zetu za kiAfrika.

Kulikuwepo na mama mmoja ambaye alikuwa akiishi na mtoto wa kaka yake. Aliishi naye zaidi ya miaka 20. Alimchukua akiwa na umri wa miaka 10 akiwa darasa la pili. Binti alimwita mama huyu shangazi. 

Aliishi nae kama mtoto wa kwake kabisa. Alimpatia mahitaji yote muhimu kwa mtoto wa kike. Kwa ujumla, alimpenda sana, sawa na mtoto wa kumzaa mwenyewe.

Ulitokea siku moja ugomvi baina ya yule binti na mtoto wa mama huyu. Katika kurushiana maneno mtoto wa yule mama alimwambia mwenzie, “kwanza wewe hapa sio kwenu, utakaa hapa mpaka lini”? Unajua tena maneno ya watoto, huwa hawana dogo. 

Iligeuka kuwa tafrani kubwa mpaka yule binti akaamua kuondoka kwenda kwa ndugu wengine. Kwa bahati mbaya, ndugu hawa hawakuwa wema kwani walimpa maneno ya kuchochea zaidi binti huyo. Badala ya kusimama kati pasipo kuegemea upande wowote na kupima ukweli uliko, waliifanya hali iwe ngumu zaidi.

Vurugu ya maneno ikawa ni kubwa sana kiasi kwamba mtu na wifi yake wakawa hawaelewani kabisa. Wifi mtu akawa anadai kuwa mtoto wake amefukuzwa na shangazi yake, ili mradi kila mtu alisema vile alivyokuwa ametafsiri mtafaruku huo. 

Mambo yote mema yaliyofanyika huko nyuma hayakuwa na maana tena, yakawa hayaonekani machoni pao. Maskini yule mama alionekana kuwa ni mbaya sana mbele za ndugu na watu wengine wanaomzunguka. 

Kisa hiki ni cha kweli, kimetokea. Kisa hiki kimeleta mtafaruku mkubwa baina ya mama wa yule binti na wifi yake. Hadi leo hii, mawifi hawa wamekuwa hawaelewani kabisa, badala yake, wamekuwa mahasidi, kisa ni ugomvi baina ya watoto wao hao wawili. 

Kuna visa vingi vinavyofanana na hiki hapa nchini. Ndugu wengi wamebaki wakilaumiana na kuwekeana uhasama kwenye mambo ambayo hayana msingi kabisa.

Simulizi hii inatufundisha kuwa makini katika kufanya maamuzi. Inatupasa kuangalia kwa undani na kutafakari hali nzima kwa ujumla wake na siyo kuchukua kisehemu kidogo na kukifanyia maamuzi. Ukosefu wa umakini unaweza ukakufikisha kwenye maamuzi mabaya, maamuzi ya chuki kama yalivyofikiwa na mzazi wa mtoto aliyekuwa anakaa na shangazi yake. 

Tunafundishwa kuwa na kiasi katika kila jambo tufanyalo. Waswahili husema, “Heri kumfadhili mbuzi, binadamu atakuudhi”. Hebu fikiria mema yote aliyokuwa anafanyiwa mtoto huyo na shangazi yake tokea alipoanza kukaa naye angali mtoto mdogo. Mema yote aliyofanyiwa huyo binti yameishia kwenye lawama tu.

Mwanadamu hana jema. Mara nyingine, watu huona kuwa heri uambiwe mbaya kuliko kutafuta wema ambao mwisho wake utakuweka pabaya. Binadamu walio wengi, hawana shukurani, bali mateke huwa ndio shukurani zao.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection

Previous
Previous

Mtoto Wa Mwenzio Mbebe Akiwa Amelala, Akiamka Huweza Kumbeba

Next
Next

Bahati Humjia Kila Mtu Kwa Wakati Wake