Mtoto Umleavyo Ndivyo Akuavyo

Simulizi
by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Mithali hii ni ya msingi sana, kuanzia pale mtoto anapozaliwa kwani tabia ya mtu inaweza kuwa nzuri au mbaya kutegemea na alivyolelewa na kukuzwa. Mfano, kama baba anakuwa na tabia ya kufokafoka na ukali uliopitiliza kila anaporudi nyumbani, watoto wake huishi kwa kuogopa muda wao wote. Pia wanaweza wakajenga tabia ya kuwa na hofu kila wakati wanapomuona baba yao. Woga ukiwazidi pia huwafanya watoto kuwa na tabia ya uongo na hata ya unafiki. Watoto wana akili sana. Wanaweza wakaamua kuwa vile mzazi wanavyomuona anataka wawe.
Baba akiwa na tabia ya ukali ukali, huwafanya watoto kumkimbia, kujificha au kujifanya wamelala kila anaporudi nyumbani.
Athari nyingine ni kupungua kwa ukaribu wa watoto na baba yao. Watoto hujenga tabia ya kuwakwepa baba zao. Maisha yao huwa ya hofu, huogopa kugombezwa kila wakati. Aidha, watoto wanakuwa hawana pa kuelezea shida zao.
Kutokana na tabia hiyo ya baba, ni rahisi kwa watoto wa kiume kuiga tabia yake. Kwa kujua ama kutokujua, wanajiaminisha kuwa tabia ya baba ndiyo tabia wanayopaswa kuwa nayo akina baba wote, hususani pale wakioa na kuwa na miji yao, pale wanapofikia hatua ya kuitwa baba mwenye nyumba.
Ili yote haya yasitokee, wazazi tunatakiwa tuache tabia za kufoka foka au kugomba gomba ovyo. Ni jukumu letu wazazi la kuwa karibu na watoto wetu. Mwalimu wa kwanza wa mtoto ni mzazi hivyo mzazi akitenda mema ama mabaya, mtoto atayaiga vile vile yalivyo. Wazazi wakiwa karibu na watoto wao, ni rahisi kwa watoto kuwaeleza matatizo wanayoyapitia. Wazazi wasio kuwa na muda na watoto wao, hujenga ukuta mkubwa baina yao na watoto. Hii ina maana hata watoto wakipata shida hawataweza kuwaeleza wazazi wao kwani hakuna ule ukaribu wa kuwafanya waifungue mioyo yao kwao pale wanapokuwa na shida ama matatizo.
Kama wazazi, tunatakiwa kutekeleza majukumu yetu vizuri kwa watoto wetu. Vile tutakavyowalea, ndivyo watakavyokuwa. Ukimlea mtoto wako vizuri, atakua vizuri na kwa maadili unayotataka ama yanayotakiwa. Hali kadhalika, ukimlea mtoto wako vibaya, bila misingi inayoeleweka, mtoto wako atakua katika misingi hiyo.
Cha msingi zaidi, wazazi ni lazima wawe na ukaribu na watoto wao ili wanapopata shida waweze kuwa na mahali pa kukimbilia kiurahisi zaidi. Mzazi anatakiwa kuwa bega la kupumzikia watoto wake kwa ustawi wa afya yake ya akili.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection