Wazazi Wana Haki Ya Kutunzwa Na Watoto Wao

Caroline Swai - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Kinachofuata ni kisa cha mama na mtoto wake wa kiume. Yaliyomo ndani ya kisa hiki yanaweza yakakuumiza sana kama una roho yenye huruma na ya kibinadamu.

Familia hii iliishi kwa furaha na upendo mkubwa. Walijaliwa kupata mtoto moja wa kiume ambaye wazazi walimsomesha vizuri na aliweza kupata kazi nzuri baada ya kuhitimu masomo yake. Maisha ya familia hii hayakuendelea kuwa mazuri baada ya baba kufariki. Kwa vile mama alikuwa tayari ni mtu mzima, mtoto wake alimpeleka kwenye nyumba ya kulelea wazee. 

Kutokana na mihangaiko mingi ya hapa na pale, kijana hakuweza kumtembelea mama yake kule aliko mpeleka, kwenye nyumba ya wazee. Alikuwa akimtembelea mara moja moja sana.

Siku moja usiku, kijana alipokea simu kutoka kwa mlezi wa mama yake pale kituoni. Mlezi alianza kwa kumwambia, "Mama yako anaumwa, njoo haraka umuone kwani hali yake ni mbaya sana”. 

Bila kuchelewa, asubuhi iliyofuata alikwenda hima kwenye nyumba ya wazee na kumkuta mama akiwa katika hali mbaya sana. Kijana alianza kulia kwa uchungu huku akisema, "Mama yangu mpenzi samahani kwa kutokuwa karibu na wewe, je ungependa nikufanyie nini?"

Mama akajibu, "Mwanangu tafadhali nunua feni ili uweke kwenye hii nyumba ya wazee, kwani hakuna feni za kutosha na wakati wa joto, inakuwa balaa humu ndani”. Mama aliendelea kwa kusema, “Pia nakuomba ununue friji na kuiweka humu ndani kwa ajili ya kuhifadhi vyakula. Mimi mamako, mara nyingi nimelala bila kula chochote kutokana na kukosa au kushindwa kuhifadhi chakula kilichokuwa kimebaki. Mara nyingi ilibidi kitupwe kwani kinakuwa kimeharibika”.

Kijana alichanganyikiwa na kumuuliza mama yake, “Mama, kwa nini ulishimdwa kunieleza haya yote kabla? Mara chache nilizokuja kukuona, hukuwahi kunilalamikia hata siku moja. Mama leo unayasema haya ukiwa unakaribia mwisho wa safari yako ya hapa duniani 🙆🏽‍♂️ Mama, mbona sikuelewi? Kwa nini umenifanyia hivyo mamangu?”.

Mama akamjibu, “Mwanangu, mimi niliweza kuishi hapa nikivumilia joto na njaa. Nachelea kusema kuwa watoto wako watakapokuleta hapa, hutaweza kuhimili hili joto na njaa iliyoko hapa. Ni hatari tupu Mwanangu. Sikuweza kukuambia mapema kwani nilitegemea una macho ya kuona”.

Kijana alisikitika na kujilaumu sana kwa uzembe wake wa kutomjali mama yake. Alikiri kuwa huu ni uzembe mkubwa kwa upande wake, uzembe wa kumtelekeza mama yake kwenye nyumba ya wazee. Mbaya zaidi akakosa hata muda wa kumtembelea. Haiingii akilini, mtoto kumtelekeza mama yake kwenye nyumba ya wazee na mbaya zaidi kushindwa kumtembelea mara kwa mara. 

Ni kweli mfumo wa  maisha unabadilika. Utandawazi mwingi, tunaiga mambo ya nje. Zamani hakukuwa na nyumba za wazee, baba, mama, watoto na hata wajukuu na vitukuu waliishi pamoja wakisaidiana humo kwa humo kwenye boma lao na uwanja uliobeba nyumba ama vibanda hivyo. Kulikuwa na upendo wa ajabu, Upendo wa kujaliana na kusaidiana. Kujaliana na kusaidiana kulikuwa ni kwa mzunguko, ili mradi kila mkazi wa boma lile hakujikuta yuko peke yake kwa wakati wowote ule. Enzi zile, wazee walilelewa ndani ya boma, na hata wazee nao waliwalea wajukuu ndani ya boma lile na hivyo ndivyo ilivyokuwa njia ya kurithisha mila na desturi zetu ndani ya boma na hatimaye, taifa lote. Leo hii, eti mtu akizeeka tu, inakuwa halali yake kupelekwa kwenye nyumba za wazee🤷🏽‍♂️. Inatisha, inasikitisha na kiutamaduni na kufuatana na mila zetu, haikubaliki hata kidogo. 

Lakini, pale itakapobidi kuwapeleka wazee wetu kwenye nyumba hizo, basi itatupasa tuwajibike kuwatembelea mara kwa mara. Tusiwaachie walezi wa kwenye nyumba za wazee peke yao kuwalea. Hao hawana uwezo wa kuwapa mapenzi waliyokuwa wakiyapata kutoka kwako. Yatupasa tukumbuke kuwa hata sisi tutakuja kuzeeka. Tujiulize, jee tungependa kufanyiwa nini tukifikia hatua hiyo ya kutengwa na wapendwa wetu? 

Hebu tukumbuke na kutafakari kidogo. Je bila mzazi, wewe ungekuwepo? Jibu ni rahisi sana. Kwa hiyo unapaswa kumtendea mzazi wako aliyezeeka vile utakavyotaka kutendewa wewe ukizeeka. Uzee haukwepeki kama Muumba wako amekujalia miaka mingi ya kuishi. Uzee unakuja kwa zamu zamu.

Ni wajibu wa kila mtu kurejesha fadhila kwa wazazi, hata wakiwa wamezeeka. Watoto wanapaswa kuwa karibu na wazazi wao, wawaheshimu, wawaonyeshe upendo na wawatunze ili wajisikie kuwa wana thamani na waone faida ya kuzaa. 

Msingojee wazazi wenu wafe na halafu mje mlie machozi ya mamba wakati mlikuwa na nafasi nzuri ya kuwaonyesha upendo wenu wote na wao wakaridhika na kufurahi kwa kuwaleta hapa duniani. Mtapata baraka za wazazi wenu mkiwapenda na kuwatunza ipasavyo.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection

Previous
Previous

Ukomo Wa Subira Yako Ndio Mwanzo Wa Husuda

Next
Next

Acha Kuishi Kwa Wasiwasi, Hapo Ulipo Bado Una Nafasi