Tuwapende Ama Tuwachukie Watu Kwa Kadri

Simulizi
by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Kupendana ni jambo la heri na la kupendeza sana.Hata maandiko yanatuasa tupendane. Lakini inabidi tuwe makini katika hilo maana huyo huyo umpendae anaweza kukugeuka siku yoyote. Hapo unaweza hata kujutia ulichokuwa umemfanyia huko nyuma. Uzoefu pia unaonyesha kuwa unaweza ukamchukia sana mtu lakini baadaye akaja kuwa wa msaada sana kwako siku ukipata shida.
Kuna kisa kimoja kilinitokea nikiwa chuoni. Kuna Mkufunzi mmoja wa hapo chuoni alikuwa hanipendi kabisa. Chuki yake ilikuwa ni ya dhahiri kabisa iliyokuwa ikilenga kunikamata kwenye somo lake ili anifelishe. Kwa bahati mbaya kwake, lakini bahati nzuri kwangu, alishindwa kutekeleza azma yake. Kimasomo, nilikuwa najiweza, lakini ilipokuja katika kutoa maksi, alionekana kuninyima stahiki yangu. Pamoja na yote hayo, sikuwahi kumfuata na kumlalamikia kwa vile anavyonifanyia.
Tulimaliza mafunzo pale chuoni, tukarudi majumbani na hatimaye kazini. Mimi nilipangiwa kwenda wizarani. Wakati nikiwa pale wizarani, yule Mkufunzi aliyekuwa akinichukia, alikuja pale wizarani. Alikuwa anatafuta jalada lake. Kwa siku mbili nzima, jalida lilikuwa halijapatikana. Kwa bahati tu, nilikutana naye kwenye korido. Nilimchangamkia tu kama vile hakijawahi kutokea kitu chochote baina yetu. Alinieleza shida yake. Kwa moyo mkunjufu, nilienda naye masijala. Tulipofika pale, nilimuomba mtu wa masijala ambaye alitusaidia mara moja. Ndani ya dakika kumi jalada lilipatikana. Mkufunzi wangu aliondoka kuendelea na shughuli zake. Hata hivyo, kabla ya kuondoka alikuja ofisini kwangu kunishukuru kwa yale niliyomsaidia. Baada ya hapo, maisha yakaendelea kama kawaida.
Lakini cha kushangaza pale wizarani kilitokea. Jamaa niliyekuwa nimemuomba anisaidie kupata lile jalada la mkufunzi, alinilaumu sana kwa kumuombea msaada yule Mkufunzi. Bila kumung’unya maneno alisema kuwa yule mkufunzi huwa ana jeuri sana na ndio maana walimsotesha kwa masaa pale masjala. Kwa upole, nilimwambia kuwa yule anayemsema ni Mkufunzi wangu. Nilimuomba amsamehe kwani binadamu hatufanani.
Tunajifunza kuwa, kama binadamu hatutakiwi kuwa na chuki kwani hatujui mambo yatakayotokea kesho. Yatupasa kupendana na kusaidiana wakati wote. Hata kama tumekoseana, kusameheana ni wajibu. Tusiweke vinyongo mioyoni mwetu. Endapo nami ningelikuwa na kinyongo na yule Mkufunzi, nisingeliweza kumsaidia. Safari yetu ni fupi sana hapa duniani. Tuyafanye maisha kuwa rahisi kuyaishi na si vinginevyo.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection