Fuata Maadili Uishi Kwa Amani

Avelina Hokororo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Avelina Hokororo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).

Amani ni kitu cha msingi sana katika maisha. Unaweza kuwa na kila kitu katika maisha yako lakini ukikosa amani moyoni mwako, yote yanakuwa ni kazi bure. 

Kuna kijana mmoja alianza kazi katika shirika fulani. Baada ya mwaka mmoja aliweza kujenga nyumba kubwa na ya kifahari. Haukupita muda sana, akanunua gari. Maendeleo yalikuwa ya haraka haraka sana kiasi ambacho yalimshitua kila mtu. Katika kipindi cha miaka miwili tangu aajiriwe alikuwa na mafanikio makubwa kupita maelezo. Pia katika kipindi hicho alioa na kujaliwa kupata mtoto. 

Maendeleo yake ya haraka haraka yaliwashangaza wengi. Watu walifanya uchunguzi na kugundua kuwa kumbe alikuwa amemuibia mwajiri wake kiasi kikubwa cha fedha. Hata Mwajiri wake tayari alikuwa anahisi kuwa lazima kuna kitu yule kijana atakuwa amekifanya. Aliyokuwa anayaona hayakuwa maendeleo ya kawaida na ya halali kwa muda mfupi aliofanya kazi.

Hali kadhalika, naye kijana alianza kujishitukia, akakosa amani. Muda wote alionekana kuwa na wasiwasi sana. Kila mtu aliuona wasiwasi wake huo. Uongozi wa shirika ulimuwekea wapelelezi kisiri siri, bila kijana kujua. Hisia za kijana zilikuwa sahihi. Kwani kwa hakika watu walikwishaanza kumshitukia. Maisha ya huyu kijana hayakuwa na amani tena kama zamani, kazini hata nyumbani. Badala ya kufurahia maendeleo yake, hali ilianza kuwa tofauti. 

Yote haya yalimpata kwa sababu ya tamaa zake. Alihisi anafuatwa na polisi, nyumbani hadi ofisini awake. Kwa hakika alikosa amani. Alianza kuwaogopa hata marafiki zake. Alihisi wanaweza kumfanyia mchongo ili akamatwe. 

Alianza kutembea na walinzi kila mahali alikoenda. Mambo yalimzidi, yalimchanganya. Hatimaye aliamua kukimbia. Aliondoka bila kuaga, yaani hata  

 mkewe hakuweza kumuaga. Aliamua kwenda nje ya nchi.

Mwajiri wake alikuja kuuza kila kitu cha yule kijana. Hali hii ilimlazimu mke wake kurudi kwao. Na huo ndio ukawa mwisho wa maraha yaliyosababishwa na wizi. Maisha ni kitendawili.

Tunajifunza nini kutokana na kisa hiki? Yatupasa tuwe waaminifu kwenye kazi zetu. Mali ya wizi haidumu hata kidogo. Tunaona yaliyomkuta huyu kijana, yanasikitisha. Kama angefuata taratibu za kufanya kazi kwa bidii na kwa uaminifu, na kutokuwa na tamaa, angefanikiwa. 

Ingemchukua muda mrefu kuchuma vitu alivyokuwa navyo, lakini vingekuwa ni vitu vyake vya halali, vitu vinavyotokana na jasho lake na siyo vya wizi. Njia za mkato za kupata utajiri hazijawahi kumsaidia mtu yeyote. Mwisho wake huwa ni mbaya. Maisha aliyokua akiishi huyu kijana pamoja na vitu alivyochuma haraka haraka, hayakuwa na raha, zaidi ya wasiwasi na mateso.

Hii pia inatokea hata kwa watoto. Kama wasipofuata maadili wanayofunzwa na wazazi, walimu, na jamii inayowazunguka, hawataishi kwa amani hata kidogo. Hali kadhalika kwa wana ndoa, kuna taratibu za kufuata ili ndoa ziweze kudumu. Yatupasa tufuate taratibu za maisha, popote tutakapokuwa ili tuweze kuishi kwa amani na raha.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection 

Previous
Previous

Mafanikio Makubwa Yana Vikwazo

Next
Next

Tuwapende Ama Tuwachukie Watu Kwa Kadri