Uhusiano wa Nidhamu Binafsi na Uchumi Katika Maisha

Caroline Swai - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Masimulizi ...

by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Alikuwepo msichana mmoja ambaye alizaliwa katika kijiji kimoja na alilelewa kwa malezi bora na akawa na nidhamu ya hali ya juu. Wazazi wake walijitahidi kwa uwezo wao wote wakamsomesha hadi darasa la tatu tu.

Binti huyo alikuwa na nidhamu binafsi kwani alikuwa mtiifu kwa kila mtu pia alikuwa na nidhamu, akisalimia anapiga magoti, anapokuwa anampatia mtu kitu napo pia anapiga magoti. Kwa ujumla alikuwa na tabia nzuri mno.

Baada ya kushindwa kuendelea na shule ya msingi kutokana na hali duni ya kiuchumi ya wazazi alienda kufanya kazi za ndani kwa familia moja ya wasomi. Baba wa familia hiyo alikuwa Profesa, watoto wake kila mmoja alikuwa na digrii mbili kutoka Vyuo Vikuu vya nje vinavyoeleweka. Ni dhahiri kwamba hii ilikuwa ni familia ya wasomi watupu.

Profesa huyo alikuwa anafundisha Chuo kimoja maarufu hapa nchini. Kama ilivyo kawaida kwa maprofesa wa Vyuo vikuu, alikuwa na jukumu la kumsimamia mwanafunzi mmoja wa chuo kikuu ambaye alikuwa anachukua digrii yake ya tatu. Hivyo kijana alikuwa anamfuata Profesa nyumbani kwake kwa ajili ya kusahihishiwa kazi zake mara kwa mara.
Profesa alikuwa akiacha maagizo kwa dada wa kazi kuwa kama kijana huyo akija amkaribishe na amhudumie kwa kumpa kinywaji anachotaka na awe anaangalia mara kwa mara ili kama amemaliza kinywaji amwoongezee. Dada wa kazi alipokea maagizo kutoka kwa bosi wake na aliyafuata barabara.

Mwanafunzi huyo alipokuja kwa mara ya kwanza nyumbani kwa Profesa dada wa kazi alimpokea kwa uchangamfu, akamsalimia kwa kupiga magoti na akamuhudumia kama alivyoagizwa, huku akipiga magoti pia. Isitoshe alikuwa anaenda kumuangalia mara kwa mara ili aweze kumhudumia zaidi.

Wakati huo huo wale mabinti wa Profesa, wakiwa na simu zao za hali ya juu na vimini vyao vya nguvu wakipita wanamsalimia yule kijana kidigitali “Hi”. Walikuwa hawapigi magoti kwani hawajazoea kufanya hivyo na baada ya hapo waliishia zao na kuendelea kuchati na kucheza game kwenye laptop zao.

Kijana yule mwanafunzi akawa anaona tofauti kubwa sana kati ya dada wa kazi na mabinti wa Profesa. Alivutiwa sana na nidhamu binafsi ya dada wa kazi.

Baada ya kumwangalia binti wa kazi kwa muda mrefu yule kijana ilibidi amweleze ukweli kuwa amevutiwa naye na angependa kumuoa. Dada alishtuka sana na kumweleza kuwa haiwezekani kwa sababu yeye amesoma hadi darasa la tatu tu na hajui mambo mengi. Badala yake alimshauri amweleze mmoja kati ya dada zake, yaani watoto wa Profesa kwa sababu wao ndio waliosoma sana kama yeye. Kijana akamjibu kuwa, amewaona hao mabinti lakini amoona kuwa hawasomeki, tabia zao siyo nzuri, hawajitambui, mavazi yao siyo ya heshima, hawajui kusalimia kwa nidhamu. Kwa ujumla, alimalizia kuwa hawana nidhamu. Bila kumung’unya maneno alisema kuwa hayupo hata mmoja kati yao anayefaa kuwa mke.

Yule kijana aliendelea kumshawishi dada wa kazi hadi akakubali kuolewa naye. Kijana alimweleza Profesa kuwa anataka kuchumbia kwenye familia yake. Aliomba kibali cha kuleta barua ya kuomba uchumba.
Profesa kusikia hayo alifurahi sana kwani alitarajia kuwa barua hiyo itakuwa inamhusu mmoja wa binti zake kwani kamwe asingefikiria kuwa msichana wa kazi ameuteka moyo wa kijana. Kwa furaha kubwa, Profesa alimkaribisha kijana nyumbani kwake kuleta barua hiyo.

Kijana alijiandaa barabara, akawa tayari kuileta barua ya kuposa kwa Profesa. Barua ilipokelewa kwa furaha sana lakini Profesa alipoifungua alikutana na jina la dada wa kazi badala ya jina la mmoja wa binti zake. Profesa alichanganyikiwa, hakuelewa maana ya kile anachokiona mbele yake. Alivua miwani yake, alidhani pengine hakuisoma vizuri barua hiyo. Akarudia kuisoma mara mbili zaidi. Lakini haikusaidia kwani haikuwa hivyo alivyokuwa anategemea. Binti wa kazi ndio alikuwa anaposwa kweli, haikuwa utani.

Kutokana na mkanganyiko huo, ilimlazimu Profesa kuahirisha hafla hiyo ya upokeaji wa barua. Kesho yake Profesa alimwita kijana akamwuliza: “mbona barua uliyoleta sikuielewa? Mbona ilikuwa na majina ambayo hayaeleweki na siyo ya mmoja wa binti zangu? Umechanganyikiwa, ama? Naona itabidi nikufanyie unasihi sasa mimi mwenyewe”.

Kijana alimsikiliza kwa umakini Profesa wake kisha akamwambia: “mimi sijachanganyikiwa hata kidogo, akili zangu ziko timamu kabisa. Ninayetaka kumposa ni huyo huyo niliyemuandika jina lake. Ninamaanisha huyo dada wa kazi za ndani hapo nyumbani kwako. Isitoshe Profesa, suala la mke ni moyo unaoamua na si vingine.

Baada ya kusikia hayo, Profesa hakuwa na la kusema tena. Ilibidi aache kuliongelea jambo hilo. Alimwambia kijana kuwa, itabidi wazazi wa dada wa kazi waitwe ili waje kupokea barua ya binti yao, kwani huo ndio utaratibu wa mila zetu.

Wazee waliitwa na kuja. Waliipokea barua hiyo na hatimaye ndoa ikafungwa.

Baada ya ndoa, bibi harusi alimweleza mume wake kuwa ana hamu ya kusoma. Mme wake alimruhusu akaanza kusoma na akawa anamsaidia pia pale nyumbani. Hatimaye aliweza kufika Chuo Kikuu na leo hii ana digrii tatu kama mume wake na wanaishi Marekani.

Kwa upande wa watoto wa Profesa hali zao ziliendelea kuwa ni zile zile za kutokuwa na nidhamu binafsi, kutojitambua, na kutokutumia vizuri fursa walizokuwa nazo. Wasichana hawa waliishi maisha yasiyokuwa na mwelekeo, walishindwa kuwatunza hata watoto wao waliowazaa wenyewe mpaka ikafikia yule aliyekuwa dada wa kazi akaamua kuubeba mzigo wa kuwatunza watoto wao.

Majukumu yale ya dada wa kazi hayakuishia hapo tu kwani alijikuta akiwatunza hata waajiri wake wa zamani, yaani Profesa na mkewe kwani walikuwa wamekwishazeeka na wakawa hawapati msaada wowote kutoka kwa watoto wao. Wazee hawa walikuwa wakipata huduma zote pamoja na huduma za afya kutoka kwa dada huyo.

Kutokana na hadithi hii ambayo ni ya kweli, tunafundishwa kuwa nidhamu kwani ni msingi wa maendeleo yetu. Huyu msichana wa kazi katika hadithi hii alifika hapo alipofikia kutokana na nidhamu yake. Lakini nidhamu hii siyo kwenye kupata wachumba tu bali ni kwa kila kitu ambacho tunakitenda hapa duniani. Nidhamu huzaa vitu vingi kama upendo, amani, furaha na heshima. ‘NIDHAMU BINAFSI NI MSINGI WA MAISHA NA MAENDELEO KATIKA KILA NYANJA ZOTE.

The Healing Hands Project

The Healing Hands project will economically empower people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community - eliminating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain the implementation of accessible psychosocial interventions in underserved communities and promote the economic empowerment of the grandmothers who have been trained in and are implementing WHO's mental health Gap Action Program. Healing Hands provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources delivered through arts, where clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection to stay up-to-date.

#MentalHealth #Grandmother #Wisdom #Wellness #mhGAP #HealingHands #Art #Culture #Tanzania

Previous
Previous

Atafutaye Hachoki, Akichoka Kesha Pata

Next
Next

Majivuno na Kiburi ni Adui wa Maendeleo