Dhuluma Haidumu

Alfreda George - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Tuko katika ulimwengu ambao kuna watu wanaishi kwa migongo ya wenzao. Watu hawa, kazi yao kubwa wanayoifanya ni kudhulumu au kutapeli wenzao. Wanaodhulumu, wanaweza wakawa ndugu au marafiki.

Palikuwa na familia moja ambayo ilipata shida ya kuondokewa wazazi wote wawili, yaani baba na mama. Watoto waliachwa wakiwa bado hawajaanza kujitegemea. Wazazi hao walijaliwa kupata mali za kutosha ambazo zingewawezesha watoto hao kusoma shule nzuri na pia kuishi maisha mazuri.

Binadamu wengine bwana ni watu wa ajabu, wanaweza kuwa ni wabinafsi na wenye roho mbaya. Badala ya kufikiria namna ya kuwatunza yatima wale, ndugu waligawana mali zote za marehemu. Waliwaacha watoto kwenye nyumba moja chini ya ulinzi wa shangazi yao.

Hali ya watoto ilianza kuwa mbaya siku hadi siku. Shangazi yao ilimlazimu aondoke pale nyumbani kutokana na kwamba hakuwa anapata msaada wowote kwa ajili ya malezi ya watoto kutoka kwa wale ndugu waliogawana mali. Shangazi alipoondoka, watoto hawakuwa na jinsi, walilazimka kuangukia kanisani kwa ajili ya kupata malezi na misaada mingine.

Waswahili husema, Mungu si Athumani, Mungu ni mwenye huruma sana. Watoto waliweza kusomeshwa, wakamaliza masomo vizuri. Mungu hamtupi mja wake. Aliwasaidia, wakapata kazi. Maisha yalianza upya kwa watoto hawa. Yalianza kuwa maisha mazuri yenye mafanikio, kiasi kwamba, ndugu bila aibu, walianza kuwatafuta watoto ili kuwaomba msaada.

Kwa wakati huo, zile mali zote walizozidhulumu zilikuwa zimekwisha. Walikuwa hawana njia yoyote ya kujikimu. Waswahili husema, njaa haina adabu. Unaweza kufikiria jinsi hawa ndugu walivyowadhulumu mali watoto hawa na leo eti bila soni wawatafute kuwaomba msaada! Haiingii akilini kabisa. Hali kadhalika, kuna usemi usemao kuwa mali za marehemu humfuata mwenyewe kule aliko na hasa pale inapokuwa mwenye haki amedhulumiwa.

Tunapata fundisho kubwa kutokana na simulizi hii. Safari yetu hapa duniani ni fupi, tena fupi sana. Yatupasa, kama wazazi/walezi kuondoa matatizo yanayoweza kutokea pale tutakapoondoka. Tutaweza kuondoa matatizo yatokanayo na dhuluma kwa kuweka kumbukumbu ya mali zetu kwa kuandika wosia kwa ajili ya kesho ya watoto wetu. Ukweli umeonyesha kwamba, mara nyingi, ndugu ni pale unapowasaidia, ukipotea ama ukiondoka inakuwa ndio basi tena. Hapo ujue udugu nao unakuwa umeondoka au umepotea.

Kuna mengi yamefanyika ya kudhulumu mali ya marehemu, pengine wengi wetu ni mashahidi. Wengi huogopa kuandika wosia, eti wanaona kama wanajichulia kifo. Hiyo ni imani potofu kabisa. Yatupasa tujivue gamba hilo. Mwaka 2023 uwe ni mwaka wa tofauti, mwaka wa kuondokana na sintofahamu zilizopo kuhusu uandikaji wa mirathi. Wosia utawaacha watoto wetu na tegemezi wetu salama. Hakuna uchuro wowote unaotokana na uandishi wa wosia.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection

Previous
Previous

Usisahau Mwanzo Wako

Next
Next

Bandu Bandu Humaliza Gogo