Chimbuko La Urafiki Baina Ya Binadamu Na Mbwa

Simulizi
by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Hapo zamani za kale, binadamu, mbwa na mbweha waliishi pamoja. Kwa pamoja, walishirikiana kufanya kazi shambani na nyumbani. Walipanda mahindi na mihogo mashambani mwao. Washirika wote watatu walilinda mazao yao ili yasiliwe na wanyama wengine.
Siku moja, binadamu aliwaambia washikaji zake mbwa na mbweha, alisema, “Tutakuwa tunalinda na shamba kwa zamu”. Mbwa na mbweha walilikubali wazo hilo na hivyo kuliunga mkono. Pamoja na kwamba wote walilikubali na kulifurahia wazo hilo la kulinda kwa zamu, bwana mbweha alilifurahia zaidi ya wote. Kimoyo moyo, mbweha alijiambia, “Sasa watanikoma, na mahindi nayo, yatanitambua”.
Siku ya kwanza binadamu alilinda, hakuna baya lililotokea na wala hakugusa mahindi kwa ajili ya kuyachoma. Siku ya pili mbwa alilinda, naye pia hali ilikuwa shwari, mahindi hayakuguswa, yalibaki salama. Siku ya tatu ilikuwa zamu ya mbweha. Naye alikwenda kulinda. Mambo yalikuwa tofauti kwa bwana huyu. Alipofika shambani, alikoka moto ili achome mahindi. Kwa bahati mbaya, upepo mkali ulivuma, na moto mkubwa ukawaka. Mbweha alihangaika kuuzima, lakini hakufanikiwa. Moto ukateketeza mazao yote.
Mbweha alirudi nyumbani kwa huzuni. Aliwaeleza binadamu na mbwa yaliyotokea. Aliwasimulia jinsi moto ulivyounguza mazao yote shambani. Binadamu na mbwa walimwuliza mbweha, “Chanzo cha moto kilikuwa nini haswa”?Mbweha alijibu kwa unyonge, “Nilikuwa nachoma mahindi“. Binadamu na Mbwa walikwenda shambani ili kujionea wenyewe uharibifu ulivyokuwa na jinsi hali ilivyo. Walishangaa kuona mazao yote yameteketea. Walisikitika sana.
Kwa hasira, binadamu alichukua rungu na kuanza kumfukuza mbweha. Mbwa naye hakumuacha. Alimkimbiza pia lakini katu, hawakumpata. Mbweha alikimbilia porini. Binadamu na Mbwa walirudi nyumbani kwa huzuni. Kuanzia siku hiyo, mbweha anaishi porini na mbwa anaendelea kuishi na binadamu kama marafiki wakubwa.
Simulizi hii inatufundisha mengi. Katika maisha yetu, kuna mambo mengi sana yanatendeka. Kuna mifano mingi ambayo inaonyesha kuwa mara nyingi tunashindwa kufanikiwa katika utendaji wetu kwa kukosa uaminifu. Watu wengi siku hizi hufanya vitu kwa kuchakachua bila hata woga. Mtu anakuwa yupo tayari kuudhalilisha utu wake kwa kujipatia mali au pesa kwa njia isiyo halali.
Pili watu wengi hawaridhiki na kile wapatacho. Imebaki tu kujiuliza, mbona yule ana kile na kile, kwanini mimi sina? Hii haiwezekani na haikubaliki kabisa. Lazima na mimi nipate. Hapo ndipo inapokuwa mwanzo wa kuharibu utiifu na uaminifu wake popote pale atakapokuwa akiwajibika. Kutokana na tamaa aliyo nayo, huanza kutekeleza uharibifu na hatima yake huwa ni kufukuzwa kazi na hata kupelekwa mahakamani.
Inapofikia hatua hii, familia na wategemezi hupata taharuki kubwa na hapo ndipo inakuwa mwisho wa maisha ya raha, yanabaki kuwa yale ya wasiwasi na taabu tupu.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection