Samaki Mkunje Angali Mbichi, Akikauka Hakunjiki

Simulizi
by Alfreda George (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Wazazi wengi tumefika mahali, tumeshindwa kuwalea watoto wetu katika maadili mazuri. Vile vile tumetoka kwenye ule utamaduni wa kusaidiana kama wazazi tofauti na enzi hizo. Zamani, mtoto alikuwa analelewa na jamii inayomzunguka, na kila mtu alilifurahia hilo. Leo imefika wakati mashtaka ya watoto yakiletwa kwako unapuuzia na kama yanahusu watoto wako, unayakataa kuwa watoto wako hawawezi kufanya hayo, kwani siyo wa aina hiyo.
Palikuwa na baba mmoja alikuwa na mabinti zake wawili wa kuwazaa. Kulikuwepo na binti mwingine alikuwa anakaa kwake, alikuwa mtoto wa kaka yake. Watoto wake walikuwa hawafanyi kazi yoyote pale nyumbani. Yule binti wa kaka yake ndiye alikuwa akifanya kila kazi hapo nyumbani. Alikuwa kama mtumishi ama mfanyakazi wa ndani.
Watoto wote watatu walipata bahati ya kupata wachumba na kuolewa. Harusi za wanae wawili zilikuwa kubwa sana. Lakini harusi ya mtoto wa kaka yake ilikuwa ya kawaida sana pamoja na uwezo aliokuwa nao. Sana sana, mtoto wa kaka yake aliagwa kwa kitchen party tu.
Shughuli ilianza pale walipofika kwa waume zao. Mabinti wale wawili hata kupika chai kwao ilikuwa ni shida. Walikuwa hawawezi kabisa. Kutokana na mapungufu hayo yaliyosababishwa na malezi mabaya, yale ya kudekezwa, ndoa zao wale wawili hazikudumu kwa muda mrefu. Mmoja alikaa kwa mume mwezi mmoja na mwingine aliweza kuhimili kwa miezi miwili tu. Hali ndio ilikuwa hivyo.
Binti aliyekuwa akifanyishwa kazi kama mtumwa, kwake ilikuwa kicheko. Ndoa yake inaendelea mpaka leo. Maskini wale wawili, kilikuwa kilio kwao, na kwa wazazi wao pia.
Kisa hiki kina fundisho ndani yake ambalo sote kama wazazi, na watoto pia, yatupasa tuzingatie. Kwa wazazi, tujifunze kuwalea watoto kwenye maadili ya kufanya kazi na kuwa na adabu kwa watu. Malezi mazuri ni muhimu sana, ili watoto wetu wakioa ama kuolewa, waweze kuwa waume ama wake wazuri. Na hata wazazi wakiondoka hapa duniani wasipate lile pengo kubwa la kushindwa kuishi bila wazazi wao.
Watoto nao wana cha kujifunza hapa. Kataeni maisha ya kudekezwa. Hata kama wazazi watakukataza kufanya kazi, bila kuwadharau, usiwakubalie kukaa bila kufanya kazi. Ukiwafuata, maisha yako yatakuwa ya taabu huko mbele. Kisa hiki ni fundisho kweli kweli kwa kila mtu.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection