Kisa Cha Kuku Na Kanga

Margaret Kayombo - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Margaret Kayombo (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Hapo zamani kuku walikuwa ndege wa mwituni. Waliishi pamoja na kanga na ndege wengine. Basi siku moja ikaja mvua kubwa huko mwituni. Kanga akamwambia kuku, nenda kwa binadamu ukaombe moto ili tuje tuote. Baridi imezidi, ni kali sana. Kuku alitii agizo la kanga. Alienda, na alipofika kwa binadamu, alikaribishwa vizuri. Binadamu alimuuliza shida iliyompeleka hapo. Kuku alijibu kwa kusema, “Nimekuja kuomba moto kwani kwetu haupo na kuna baridi sana.

Kwa ukarimu wa binadamu, alizidi kumkaribisha zaidi kwa kumpa vyakula vizuri. Kuku aliguswa na ukarimu huo, aliona kuwa binadamu ni watu wazuri na pia wanastarehe sana. Mwishowe kuku alijisahau alichotumwa. 

Kule mwituni, kanga alipoona kuku amekawia kurudi, alimtuma jogoo aende kumhimiza ili arudi haraka. Jogoo naye alipofika, alikaribishwa vizuri, akapewa vyakula tele. Alipoangaza huku na kule, alimuona kuku amestarehe, kaupiga usingizi mzito ikiwa ni dalili kuwa amesahau kabisa sababu iliyompeleka pale. Ni kwamba, alikuwa hana habari kama katumwa na kanga kule porini.

Kuku alipoamka, jogoo alimhimiza apeleke moto kule mwituni. Kwa kunogewa na mahali hapo, kuku alimjibu jogoo kuwa harudi tena mwituni maana binadamu wamemtendea mema mengi. Alizidi kwa kusema, “Nirudi mwituni nikafanye nini”? Badala yake, kuku akazidi kumpa jogoo chakula alichobakiza ili ale. Hatimaye, naye jogoo, mwisho alijikuta ameingia kishawishini, kwenye mtego, naye akakataa kurudi mwituni.    

Hivi mnajua sababu ya kuku kunywa maji akitizama juu? Watu husema kuku hufanya hivyo kama ishara ya kumshukuru Muumba aliyewajalia kupata riziki kutoka kwa binadamu. Tunaweza tukasema binadamu ni wema lakini wana mapungufu wakati mwingine. Siku moja walikuja wageni nyumbani kwa binadamu. Ilitokea kwamba binadamu alikuwa na chakula, lakini hawakuwa na kitoweo. Maamuzi yalifikiwa haraka haraka, yalikuwa ni kumchukua kuku na kumchinja ili wapate kitoweo cha wageni. 

Binadamu walimkamata kuku, naye alilia, si mimiiiiiii ! Si mimiiiiiiiii ! Lakini wapi, kilio chake kiliangukia patupu, kuku akachinjwa. Jogoo kuona mwenziye anachinjwa, alipiga kelele, naye akalia Koko! Likooo! ikiwa na maana kuwa “Kuku wewe umenidanganya.”

Kanga naye mwituni alichoka kusubiri. Basi naye akaja karibu na nyumba ya binadamu, akapiga kelele, “Kuku weee! Kuku weee! Nilikuomba uende u kachukue moto!” Lakini ilikuwa kimya, hakusikia sauti yoyote na alipozidi kuita, jogoo akamjibu, “Ya kale hayakoooo!Usiingie ujinganii…” Kanga aliposikia hivyo akajua kuwa hawa hawarudi tena, akarudi zake kwenda mwituni. 

Kutokana na hili somo tunajifunza mengi kama vile kuacha kufuata mkumbo katika maamuzi. Yatupasa tutumie hekima zetu binafsi katika maamuzi yaliyo sahihi. Baadhi ya vijana huingia kwenye matatizo mengi kutokana na kufuata mkumbo. Wengi huwa hawachukui muda wa kutafakari, huwa hawaangalii athari zinazoweza kutokea baadaye. Vijana wengi huingia kichwa kichwa tu kwenye mambo wasiyoyajua. Mwisho wake huwa ni mbaya. Fikiri, kabla ya kutenda. Usifanye jambo kwa kukurupuka, itakugharimu baadaye. Ule usemi wa Majuto ni Mjukuu, utakuhusu usipoangalia.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection

Previous
Previous

Binadamu Ana Nyuso Mbili, Kaa Nae Kwa Akili

Next
Next

Samaki Mkunje Angali Mbichi, Akikauka Hakunjiki