Ukishindwa Hili Leo, Kesho Utashinda Lile

Grace Mshanga - Wisdom&Wellness Counselor (TEWWY)

Simulizi

by Grace Mshanga (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).

Wakati sisi tunasoma shule ya msingi, ilikuwa ni madarasa manne tu, yaani la kwanza hadi la nne. Enzi hizo walizingatia sana umuhimu wa kila darasa kuwa na wanafunzi wasiozidi arobaini na tano. 

Alikuwepo mwanafunzi  mmoja wa kike ambaye alikuwa amerudia darasa la kwanza miaka miwili. Kutokana na hali hiyo, walimu waliamua kumpeleka darasa la pili ambako alikutana nasi. Hata hivyo ilibidi arudie tena mwaka darasa la pili wakati sisi tulipoingia darasa la tatu, yeye alibakia darasa hilo hilo la pili.  

Tulipoingia darasa la nne, walimu waliamua tena aingie darasa la tatu. Shida kubwa ya binti huyu ni kwamba alikuwa hawezi kuandika na kuhesabu kabisa. Hivyo baada ya walimu kutumia njia zao zote walizozijua pamoja na maarifa yao yote na bado ikashindikana, walilazimika kumuachisha shule kabisa, akiwa darasa la tatu. 

Wazazi wa binti huyu walipenda sana binti yao asome. Walijaribu sana kumfanya asome lakini haikuwezekana kabisa. Ikumbukwe kuwa, wazazi wa huyu binti walikuwa ni watu matajiri sana hapo kijijini kwetu. Baba yake alikuwa na cheo kikubwa serikalini. Familia yao ilikuwa inapendwa sana pale kijijini. Pia binti huyu alikuwa ana adabu nzuri na aliwaheshimu watu wote, wakubwa kwa wadogo. 

Binti alizidi kukua na kuwa mrembo. Tabia ya kuwaheshimu watu ilitambuliwa na kila mwana jamii pale kijijini. Hali kadhalika, aliendelea kuwa mwenye adabu. Kwa hakika, alipendwa na kila mtu.

Vijana wa hapo kijijini, watoto wa matajiri na wa maskini pia, walijaribu bahati zao kwa kila namna kutaka kumchumbia. Lakini binti huyo hakumpenda hata mmojawao. Wazazi nao wakajaribu kumshawishi lakini alikataa, akisema bado hajampata yule anayempenda. 

Ilipita muda akatokea kijana mmoja, ambaye kwake yeye binti aliona kuwa ndiye chaguo lake. Pamoja na kwamba kijana  hakuwa wa kabila lake, binti aliamua kuolewa naye. Hilo halikuwa tatizo kwake, kama wahenga wasemavyo, ‘Kipenda roho, kula nya mbichi’.

Sisi tuliokuwa tunasoma naye huko shule za msingi, tuliendelea na masomo hadi kuhitimu vyuo vikuu na kuajiriwa. Baada ya kufanya kazi kwa miaka kama sita hivi nilikutana naye. Nilipomuona nilishangaa kutokana na hali yake nilivyoiona. Alionekana kuwa na hali nzuri na alikuwa na afya njema. Uzuri wake ulikuwa umezidi, alionekana kuwa mrembo zaidi. 

Katika maongezi yetu, tulielezana mengi. Kila mmoja wetu alikuwa na shauku ya kujua ya mwenzake. Aliniambia kuwa ana watoto saba na kwamba walishajenga nyumba yao ya kudumu. Zaidi ya mafanikio hayo, watoto wao wanne walikuwa wanasoma shule za English Medium, na wengine watatu walikuwa shule za awali (chekechea). Hata mimi nilimweleza yangu niliyokuwa nayo. Ilikuwa ni furaha na shangwe tupu kubadilishana yaliyojiri tokea tumeachana miaka hiyoo ya huko nyuma. 

Simulizi hii inatuonyesha kuwa mtu anaweza kushindwa na hili leo lakini kesho akashinda lingine. Pamoja na kwamba huyu mama alishindwa kusoma na kuandika kabisa, bado aliweza kupata maendeleo kwenye upande mwingine. Mungu alimjalia watoto wengi na kumpa maendeleo makubwa, kama ya kujenga nyumba ya kudumu na kusomesha watoto wao kwenye shule nzuri. 

Ushauri kwetu sote ni kwamba, ukishindwa na hili leo usikate tamaa hata kidogo. Unaweza kuja kushinda lingine kesho yake ama siku nyingine. Mungu wetu yuko kazini kila siku. Maisha yetu hayagandi mahali pamoja, yanaendelea yakibadilika kila uchao. Ni mwiko kukata tamaa ili mradi bado tunaishi hapa duniani.

The Healing Hands Project

The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection

Previous
Previous

Hekima Ni Jambo La Msingi

Next
Next

Huwezi Kupanda Ngazi Ya Mafanikio Ukiwa Umeweka Mikono Mfukoni