Anayetembea Kwenye Matope Yampasa Asafishe Miguu Yake

Simulizi
by Caroline Swai (Wisdom&Wellness Counselor - TEWWY).
Hapa duniani kuna aina nyingi za barabara. Kuna barabara zile za lami, moramu na vumbi. Ikitokea umetembea kwenye barabara ya vumbi na mvua ikawa imenyesha, utakanyaga matope.
Hivyo itakubidi uwe unasafisha miguu yako mara kwa mara wakati wa safari kutokana na tope litakalokuwa linanasa kwenye miguu yako. Tope likinasa hutaweza kutembea vizuri kwani miguu itakuwa mizito na hivyo kufanya safari yako kuwa ngumu.
Hapa duniani, katika maisha yetu tunapitia mapito mengi au njia nyingi ambazo zina matope. Mara nyingi inakuwa vigumu kuzuia au kukwepa matope hayo ili tusichafuke. Matope haya tunaweza kuyafananisha na mambo ambayo tunayapitia hapa duniani.
Kuna watu wengine wanaweza wakakuchafua kwa kukusema vibaya. Kuna wakati watakusingizia ama kukuzulia mambo mengi ya uongo na yasiyofaa ambayo hujatenda wala huwazii kuyatenda. Wao nia yao kubwa ni kukufanya uonekane mchafu, mtu usiyefaa kwenye jamii hata uonekane huna maana hapa duniani.
Endapo utapakwa matope au utachafuliwa na wabaya wako, lazima uwe imara. Yakupasa ujitengenezee uhalali au utamaduni wa kujisafisha kwa lengo la kuyaondoa kabisa matope hayo ili uweze kusonga mbele. Unaweza kuyaondoa matope hayo kwa kutokaa kimya, bali kuongea ukweli na kujitetea kwa kila hali.
Katika maisha, ni kawaida kuwa ukisingiziwa jambo na ukakaa kimya, watu wataona kuwa hilo jambo ni la ukweli. Hivyo ni muhimu ujitetee ili ukweli ujulikane. Kamwe usikubaliane na msemo uliozoeleka usemao, “Kubali Yaishe”, kwani huo hautakuwa ufumbuzi wa kuweka mambo bayana. Ukichafuliwa, inakupasa ujisafishe.
Tunatahadharishwa kutokubali kupakwa matope kwa kuonewa au kusingiziwa mambo tusiyoyatenda. Pale itakapotokea kuwa tumepakwa matope ama tumesingiziwa, itatupasa tujisafishe kwa kujitetea ili kuweka mambo sawa. Maisha yanatakiwa yaendelee mbele na hasa ikizingatiwa kuwa safari yetu ni fupi sana hapa duniani.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection