Mkataa Kwao Mtumwa

Simulizi
by Avelina Hokororo (Wisdom&Wellness Counselor – TEWWY).
Msemo huu unaweza ukamaamisha mtu anayekataa kabila lake, anayekataa utaifa wake na akaweza kuwakataa hata wazazi na ndugu zake pia.
Mtu anaweza akafanya hivyo kutokana na sababu mbali mbal. Sababu mojawapo inaweza kuwa ni aina ya chakula chake cha asili kinacholiwa kwao. Kule atokako wanakula chakula ambacho mikoa mingine hawali na pengine ni chakula kinachodharauliwa na makabila mengine. Au pengine ukoo wake ni wa hali ya chini na hivyo asingependa ahusishwe nayo.
Huenda katika familia yake, ni yeye tu ndiye alipata bahati ya kusoma na kupata kazi. Badala ya kumshukuru Mungu kwa kujaliwa kupata kazi, yeye amekuwa na tabia ya kumkufuru Mungu.Hizo ni sababu chache kati ya nyingi ambazo watu hujikataa na kuwa watumwa wa fikra.
Kuna kijana mmoja alibahatika kusoma kupitia nguvu na upendo wa wazazi wake. Wazazi hawa walikuwa wakishujishulisha na biashara ndogo ndogo. Baba alikuwa akichoma mkaa na mama alikuwa akichoma vitumbua na maandazi ili kijana wao aweze kusoma na kupata elimu.
Hakika Mungu aliwasikia wazazi hawa na kuwajaalia hitaji la mioyo yao. Kijana alisoma na kufika hadi Chuo Kikuu na pia alibahatika kupata kazi nzuri. Baada ya muda kidogo, kijana aliweza kuwa na nyumba yake nzuri. Hali kadhalika aliweza kununua gari kwa ajili ya usafiri wake. Pia aliweza kuoa.
Kule nyumbani wazazi wake na ndugu zake walibaki kwenye maisha yale yale duni. Nyumba yao ya kuishi ilikuwa ni ya udongo iliyoezekwa kwa nyasi. Biashara zao ziliisha. Mali asili waliingilia kati na kukataza uchomajii wa mkaa, ambayo ndiyo ilikuwa biashara kubwa ya baba. Hivyo akawa hachomi tena mkaa.
Biashara ya mama ilipungua kwa kasi maana na umri ulikuwa umeenda. Alikuwa hana nguvu kubwa ya kukanda unga wa maandazi.
Siku moja wazazi hawa waliamua kumtembelea mtoto wao baada ya kukosa mawasiliano kwa muda mrefu. Walipelekwa na mwanakijini mwenzao ambaye anaishi huko mjini. Mtoto wao aliwapokea lakini alishindwa kuwatambulisha kwa mke wake na hata kwa rafiki zake. Aliwaona kuwa hawana hadhi ya kutambulishwa kwa jinsi hali yao ilivyokuwa. Bila aibu aliwaambia mke na rafiki zake kuwa wazazi wake walifariki siku nyingi na kwamba hawa ni wazazi wa yule jamaa aliyewaleta, kwa kuwa kwake alikuwa hana mahali pa kuwalaza. Hiyo ndiyo ilikuwa sababu ya kumuomba walale kwake.
Mke wake na marafiki zake waliamini uongo wake huo. Hivyo waliwekwa kwenye chumba cha nje na kupelekewa kila kitu kule kule na mfanyakazi wao. Wazazi walitambua unyanyapaa ule, hivyo waliomba nauli na wakaondoka na manung'uniko.
Baada ya siku si nyingi yule bwana alifukuzwa kazi kwa makosa yasiyoeleweka. Mke wake alimkimbia. Alianza kuuza kitu kimoja kimoja ili ajipatie riziki maana jitihada za kutafuta kazi hazikuzaa matunda. Alipomaliza kuuza nyumba na vitu vyote, aliishiwa cha kuuza. Basi aliamua kurudi nyumbani ili akaombe msamaha kwa wazazi wake. Cha kusikitisha, alikuta wazazi wake wote waliishafariki kitambo.
Hakuweza kurudi mjini tena, alilazimika kuishi kwenye nyumba ile ile ya wazazi wake., nyumba ambayo ingekuwa haina hadhi kwake. Kwa hakika, alichanganyikiwa.
Ndugu zake walimsaidia kimaisha, walimlea kama kichaa.
Hicho ndicho kiburi cha elimu.
Tunajifunza mengi sana katika simulizi hii. Yatupasa tuwe wanyenyekevu katika hali yoyote iwayo. Wazazi ni wazazi tu na watakuwa hivyo daima. Kamwe tusiwadharau wazazi na tusidharau kule tulikotoka. Kwako ni kwako tu, hata kuweje.
The Healing Hands Project
The Healing Hands empowers people to achieve financial autonomy by building entrepreneurial skills and embedding skills transfer within the community – alleviating poverty as a driver of ill mental health. Funds raised from the jewelry will help sustain free mental health services in underserved communities and promote the economic empowerment of trained grandmothers who implementing #WHO #mhGAP evidence-based psychosocial interventions. The project provides interpersonal counseling, group talk therapy, and psychoeducation resources, referrals, advocacy and awareness raising delivered through arts. Clients learn to handcraft traditional beaded jewelry as a marketable skill. Follow us @TEWWYWisdom @WisdomWellnessCollection