Bora Lawama Kuliko Fedheha!

Christina Mande
Wisdom&Wellness Counselor

Kizinga, Dar-es-Salaam

Lawama ni ile hali ya mtu kulalamikiwa ama kushutumiwa kwa kukosa ushirikiano au kupuuza mambo angamizi kwenye jamii. Na fedheha ni ile hali ya kudhalilika au kuaibika kutokana na kutenda jambo lisilokubalika kwenye jamii.

Msemo huu unatufundisha sisi binadamu, tuishi maisha yaliyo ndani ya uwezo wetu. Hatutakiwi kulazimsha mambo ili tu kuwafurahisha wengine. Kwa mfano siku hizi kuna akina dada wengi mitaani ambao wana vikundi vyao vinavyoitwa vikundi vya kutunzana. Unaweza ukawakuta wengine hawana kitu chochote cha kuwawezesha kuingia kwenye mchezo kama huo. Pale wanapokuwa wameshirika kwenye kutunzana huko huwa inawawia vigumu kurudisha fadhila pale watakapotakiwa na wao kuwatunza wenzao kufuatana na utaratibu wao. Watu hawa huwa wako tayari kwenda kuchukua mikopo inayoitwa kwa jina la kutisha la “kausha damu” ili mradi tu waweze kuwafurahisha rafiki zao kwa kuwatunza vitu vya gharama. Lengo lao kubwa ni kutaka kuonekana kuwa nao “wamo” kwenye makundi ya walio nacho. Hii ni hatari sana kwa maisha yao kwani wanakuwa hawaishi kiuhalisia wa maisha yao.

Endapo watajiingiza kwenye mikopo, pale watakaposhindwa kurejesha, huwa ni balaa kubwa. Kifuatacho huwa ni
kufilisiwa na hata kile kidogo walichonacho. Kilichobakia ni kupata aibu
na fedheha kubwa kwenye jamii inayokuzunguka.

Hapa tunajifunza kuwa ni bora watu wakulaumu kwa kutoshirikiana nao kwenye mambo yasiyo kuwa na maana kuliko kujiingiza kwenye mambo usiyoyaweza ili mradi tu tusifiwe na wewe uonekane iko kwenye jamii hiyo. Mwisho wa hayo yote huwa ni fedhea na aibu kubwa. Yatupasa tuishi kufuatana na uwezo wetu tuliojaliwa na Muumba.

Previous
Previous

Wembe Ni Mkali Lakini Haukati Mti, Shoka Ni Kali Lakini Haikati Nywele.

Next
Next

Njia Ya Muongo Ni Fupi!