Ndege Hai Hula Mchwa, Akifa Naye Huliwa Na Mchwa.

Christina Mande
Wisdom&Wellness Counselor

Kizinga, Dar-es-Salaam

Ndege ni mkubwa kwa umbile ukimlinganisha na mchwa na sisimizi ndio maana anaweza kuwala wadudu hao bila shida. Lakini ndege huyo huyo akifa biashara inabadika. Akifa anakuwa hana ubabe tena, hivyo mchwa na sisimizi nao wanapata ubavu wa kumla.

Mzunguko huu wa ndege, mchwa na sisimizi uko pia kwa binadamu. Kwa mfano mtu anaweza kuwa ana uwezo mkubwa kiuchumi au kuwa na madaraka makubwa serikalini ama mahali popote. Mara nyingi watu hawa wenye madaraka wanaweza wakatumia uwezo na madaraka yao kukandamiza na kunyanyasa walio chini yao. Na wengine huwatumikisha wale wa chini kwa ujira mdogo bila hofu yoyote.

Ikumbukwe kuwa maisha hubadika, leo una uwezo mkubwa kiuchumi au kimadaraka lakini kesho uchumi unaporoka na madaraka unakuwa huna tena. Yawezekana kabisa hao waliokuwa chini yako wakiwa wanyonge wako, sasa wanakuwa juu yako. Hebu jaribu kufikiri, utajisikiaje?

Hivyo kama binadamu, yatupasa tusiishi kwa kuoneana kama ndege na mchwa na sisimizi kwa sababu hatujui kesho yetu itakuwaje. Maisha ni mzunguko na ndivyo Muumba wetu alivyoyaweka. Hakuna mdudu/mnyama au binadamu yeyote aliyeumbwa kutesa ama kuteseka milele. Lazima tuzingatie hayo.

Previous
Previous

Maamuzi Yako Leo Ndiyo Mlango Wako Wa Kutokea Kesho!

Next
Next

Pakacha Kulivunja Nafuu Ya Mchukuzi!