
Kidole Kimoja Hakivunji Chawa
Katika maisha ushirikiano ni nguzo kubwa sana kwenye nyanja yeyote. Mahali pa kazi pakikosa ushirikiano kunaweza kutokea vurugu inayoweza kusababisha hasara kubwa. Kitakachoonekana ni mashindano ya mara kwa mara ambayo hayana tija.

Umaridadi Huficha Umaskini
Umaridadi utakuwezesha kuwa na muonekano unaotaka. Haijalishi kazi ufanyayo bali cha msingi ni kupenda kile unachofanya. Usiruhusu kazi unayofanya iwe kikwazo katika mwonekano unaotaka uwe.

Tambua Adui Anayekutafuna
Mtesi wa maisha yako ni wewe mwenyewe ndiyo maana wanasema angalia habari zako kwanza kabla ya kutafuta mambo ya wenzio. Yakupasa kufahamu kwamba unatakiwa kuyatatua yale yanayo kuhusu wewe mwenyewe kabla hujaanza kutatua ya watu wengine.
Chakula cha Mchana Hakikosi Kuni
Kuni ni nishati itokanayo na miti. Nishati hii hutumika kupikia chakula, kuchomea matofali, au kuota kwenye maeneo ya baridi kali.

Kinywa ni Jumba la Maneno
Kinywa kinahusisha mdomo na ndani yake kuna ulimi. Hapo ndipo yanapotokea maneno chanya na hasi, mazuri na mabaya. Tunasema ni jumba la maneno kwa sababu maneno yote hutokea hapo.

Bora Mchawi Kuliko Mfitini
Dunia imejaa fitina za kila aina. Wako watu ambao kazi yao kubwa ni kufitinisha au kuchonganisha watu. Mara nyingi, hali hii hutokana hasa pale wanapoona fulani anaelewana vizuri na fulani. Watatafuta kila njia ili wawakosanishe.

Chui Hakumbatiwi
Fikira za mwanadamu huwa hazina ukomo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba binadamu ana mambo mengi ya kuwaza wakati wote. Kuna mambo tunayawaza yakiwa ni ya hatari kwetu na ya kuhuzunisha pia. Mambo ya kuhuzunisha huwezi kuyakumbatia. Mambo hayo ni kama uvivu, wizi, kutowajibika, kusengenya na kusema uongo. Ukitaka kuwa na amani, inakupasa ujitenge na mambo hayo, hii ni kwa ajili ya ustawi wako mwenyewe.

Usisamehe Kama Hauko Tayari Kusahau
Msamaha ni jambo la kiungwana ambalo mtu anafanya au anatakiwa kufanya kwa mtu ambaye amemkosea au kumuudhi katika jambo lolote. Kwa watu wengi, kuomba msamaha huwa siyo jambo rahisi, huwa kuna ugumu fulani. Ugumu huu hutokana na ile tabia ya kushindana na kujihesabia haki.

Epuka Wasengenyaji
Wasengenyaji ni watu wasiokuwa na kazi na huwa wanawasema wenzao bila sababu ya msingi. Watu hawa ni wa hatari sana kwani huwa wanatumia muda wao mwingi katika kujadili maisha ya watu wengine. Tunashauriwa kujiepushe kujenga urafiki na watu kama hao.

Fimbo ya Mbali Haiui Nyoka
Wanadamu tumeumbwa kusaidiana. Usemi huu unatufundisha umuhimu wa kuishi vizuri na jamii inayotuzunguka. Hii ina maana kuwa ukipatwa na janga lolote, jirani yako ndiye atakuwa wa kwanza kuja kukusaidia na kukufariji. Haijalishi ni ndugu ama laa.

Tusilaumu Wala Tusihukumu Wengine
Lawama ni kitendo cha kumlaumu mtu kutokana na makosa aliyokufanyia kwa kukusudia au bila sababu. Watu wengi hawapendi kufuatilia mambo kwa kina ili kupata ukweli ambapo humfanya mtu aamini mambo bila kuchunguza. Hali hiyo husababisha wengine kuumia ndani kwa ndani bila kupewa nafasi ya kusikilizwa.

Mwenda Pole Hajikwai
Maisha ni safari ndefu sana yenye milima na mabonde. Mara nyingi kupanda mlima huwa kuna ugumu wake na kunahitaji umakini sana ili usikwame njiani ukashindwa kufika juu kunako lengo lako.

Maisha Ni Milima Ya Kupanda Na Kushuka
Maisha ya mwanadamu yana utaratibu wake wa kupanda na kushuka. Hata ingekuwaje, hakuna mtu anayeweza kuibukia kileleni bila kwenda kwa hatua. Utaratibu uliopo ni kupanda hatua moja baada ya nyingine ndipo ufike kileleni.

Jipe Muda Wa Kufurahia Yale Uliyobarikiwa
Ni jambo la kawaida kabisa kwa binadamu kupenda kuwa na furaha siku zote za maisha yake. Lakini yatupasa tuelewe kuwa furaha hiyo haipatikani ki urahisi. Inakupasa kuhangaika na kujishugulisha ili uweze kutimiza matakwa yako na ufurahie matunda ya kazi zako. Lakini badala ya kujishughulisha, inafikia wakati tunaangalia fulani kafanya hiki au kile na ndio maana kafanikiwa zaidi. Tunafikiria kuwa mafanikio yake huenda yalipatikana kiurahisi. Hatuchukui muda kuchunguza alikotoka hadi akafikia hapo alipo. Tunafikiri yote aliyonayo aliyapata kiurahisi tu.

Mtoto Wa Mwenzio Ni Wako
Mtoto ni mwanadamu mwenye umri mdogo ambaye hajafikia kuwa mtu mzima. Kutokana na umri wa mtoto huyu kuwa mdogo, anapaswa apewe malezi bora kama vile, chakula, malazi, malezi, elimu na haki zake zote za kimsingi.
Mafanikio Ya Mtu Hutegemea Uwezo Wa Kufikiri Na Kutafakari
Mafanikio ya mtu yeyote hapa duniani hutokana na bidii, kujiamini, kiwango na uwezo wake wa kufikiri na kutafakari. Aidha, wengine hupoteza muda wao kuwaza jinsi watu wengine wanavyowaona, wanavyowafikiria, wanavyowatafakari na wanayowawazia.Hata hivyo inabidi kujua kwamba, ili uweze kufanikiwa katika maisha, kamwe usitumie muda wako kuwaza kuwa nikifanya hivi wengine watanionaje ama watanifikiriaje. Inakubidi wewe ufanye shughuli zako kwa kujiamini. Ili mradi unachofanya kiwe ni sahihi mbele ya Mungu na mbele za binadamu wenzio.Kwa kuwa na mtizamo huo chanya, mawazo ya watu wengine hayataruhusiwa kuitawala akili yako. Mtazamo chanya utakufanya usimame imara kwenye kile unachokiamini na hatimaye, utapata mafanikio.Hapa tunapata funzo kuwa, kamwe tusiumize vichwa vyetu na kuchukua muda mwingi kuwafikiria watu wengine wanachowaza juu yetu. Jiulize wewe unawaza nini kuhusu wao pamoja na kwamba hata wewe siyo kazi yako kuwawazia wengine. Wewe jali kazi na maisha yako na mambo yanayokuhusu. Acha kuwafikiria wao kwani mambo yao wewe hayakuhusu.

Asiye Uliza Hana Cha Kujifunza
Kuuliza ni tendo la kutaka kufahamu au kujua jambo ambalo hulijui au hulifahamu. Inawezekana pia hilo jambo unalifahamu lakini huna hakika kama hicho unachokifahamu ni sahihi. Kwa hiyo unatafuta kuelekezwa zaidi na mtu mwingine.

Siyo Kila Unalofanya Litampendeza Mwingine
Katika jamii inayotuzunguka siyo kila mtu ni mzuri kwako, laa hasha. Wabaya wapo wengi pia. Kuna watu ambao hawapendi mafanikio au maendeleo ya watu wengine. Mara nyingine unajikuta kwenye jamii ambayo kila wakati unapingwa na kudharauliwa. Kila utakachofanya unakosolewa bila sababu ya msingi. Binadamu kwa kweli ni kiumbe wa ajabu.

Zimwi Likujualo, Halikuli Likakwisha
Katika maisha, watu tunaishi kwa kufahamiana na kujuana. Kuelewana huko kuko katika tabaka mbalimbali, mathalani, kwenye jamii zetu, familia zetu na hata kwenye makundi maalumu. Hata kwenye sehemu za kazi matabaka haya ama makundi haya hujitokeza sana. Huwa kuna upendeleo dhahiri unaotokana na kufahamiana, hilali hiyo ipo.

Debe Tupu Haliachi Kutika
Tupo katika ulimwengu wenye mambo mengi yanayotuzuguka. Kwa kawaida, maisha yetu yako katika makundi makundi. Yapo makundi yenye uwezo mkubwa, yapo yale yenye uwezo wa kati, hali kadhalika yale ya kawaida. Kundi hili la mwisho ni lile ambalo inawezekana hata riziki ya siku ni ya kubabaisha. Inaweza hata siku ikapita bila ya kuwa na chochote.